The path to success

Wednesday, 1 February 2012

MGOMO HUU WA MADAKTARI NI JANGA KWA TAIFA



Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Nkopi akifafanua jambo wakati wa mkutano mkuu wa madaktari nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha na Richard Mwaikenda.

TUMSHUKURU Mungu kwa kutuweka hai leo tukiwa na uzima na afya tele, lakini tukimuomba atuepushie balaa katika nchi ili mgogoro wa madaktari kama unaisha basi usijirudie kwa kuwa unatesa watu wanaougua.
Baada ya kusema hayo niende moja kwa moja kwenye mada inayohusu mgomo wa madaktari ambao kwangu naona haina maana kwa mamlaka zinazohusika kungoja matabibu wagome ndipo wakubwa waanze kuwaboreshea au kuwalipa masilahi yao.
Kiukweli si maadili kitaaluma kwa madaktari kugoma kufanya kazi, kwa kufanya hivyo wanayaweka maisha ya wagonjwa hatarini  japo wana hoja za msingi katika madai yao.
Hakuna asiyejua kuwa udaktari na uuguzi ni miongoni mwa kazi ambazo zinahitaji uadilifu na utu wa hali ya juu zaidi ya kitu chochote kwa kuwa ni kazi inayohusu uhai wa mtu na afya inayomuwezesha kuzalisha mali kwa faida yake na taifa kwa ujumla.
Kwa sababu hiyo, serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kuhakikisha kuwa masilahi ya wataalamu hao yanazingatiwa ili kuepusha migomo inayoleta madhara makubwa, kama vile wagonjwa kufa kwa kukosa huduma ya tiba, hivyo kupunguza nguvu kazi ya taifa.
Ndugu zangu, kusema kweli madaktari na manesi ndiyo waliopewa dhamana ya uhai wetu hapa duniani, hivyo mtu anapoumwa uhai wake huwa mikononi mwao.
Mgomo wa madaktari japokuwa una masilahi kwao lakini  kwa  wananchi wa kawaida ambao hawana uwezo wa kwenda katika  hospitali za kulipia hapa nchini au India na kwingineko ni pigo kubwa kwao  kwani kipindi chote cha mgomo huwa katika hatari ya kifo.
Kama ulibahatika ukaona wagonjwa walivyokuwa wakiteseka wakati wa mgomo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, utagundua kwamba kitendo cha kugomea kazi ni cha uuaji japokuwa ni cha kudai masilahi yao.
Katika wodi moja ya Sewahaji kwa siku moja wagonjwa saba walipoteza maisha, idadi ambayo ni kubwa sana japokuwa inawezekana hata madaktari wasingegoma wangeweza kufariki dunia, lakini ukweli ni kwamba mgomo umeonekana umechangia wagonjwa wale kufariki.
Katika chumba cha upasuaji, wengi wa wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma hiyo walishindwa kuipata na kwa vyovyote maisha yao yalikuwa hatarini kwani wagonjwa walipigwa tarehe ya kupewa huduma hiyo.
Ki ukweli, kama hujui madhara ya kuumwa tembelea hospitali hasa za serikali utajua nini nakisema. Mgomo wa madaktari unafanya wagonjwa waathirike kisaikolojia na kuwafanya wajione hawawezi kupona tena, hivyo wengine kufariki kutokana na kufadhaika.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba mgomo huo umesambaa na kuenea hadi hospitali zingine kama vile ya Ocean Road inayotibu wagonjwa wa saratani iliyopo Dar, Hospitali za Mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza na Morogoro.
Hili ni janga kwa sababu wananchi walio wengi ambao hawana kipato cha kuwawezesha kutibiwa katika hospitali za kulipia, kimbilio lao ni kwenye hospitali za serikali ambako madaktari wanagoma.
Naiomba serikali iliangalie hili kwa upana na linaloweza kufanyika kwa haraka lifanyike ili madaktari warejee kazini wakaendelee na kazi kama kawaida wakati suluhisho la kudumu likitafutwa ili adha hii tusiweze kuishuhudia tena katika nchi yetu.
Ikibidi kusitisha baadhi ya huduma ambazo zinaweza kungojea, serikali ifanye hivyo ili madaktari walipwe na waende kuokoa wagonjwa. Kwa kuendelea na mgogoro huu wanaoumia ni wananchi masikini ambao hawana uwezo wowote wa kwenda kutibiwa katika hospitali za kulipia.
Tuliona jinsi posho za wabunge ya shilingi 200,000 kwa siku ilivyotaka kupitishwa haraka sana na Spika Anne Makinda alivyoitetea kwa nguvu lakini hili la madaktari mtetezi wao ni nani ndani ya serikali ili kama madai yao ni halali wakashughulikiwa?
Watu walionya awali kuwa kama wabunge wana hali ngumu wanapokuwa pale Dodoma na hata watumishi wengine wa serikali  walio katika sekta mbalimbali nao watapenda kuongezewa posho, kwani maisha yao ni magumu na matokeo yake ni haya tunayoyashuhudia leo.
Waziri wa Afya, Dk. Hadji Mponda nilimsikia wiki iliyopita akiwaambia madaktari kuwa suala la kushughulikia mishahara yao ni kubwa ambalo linahitaji jitihada na akasema kuwa ndiyo maana milango ipo wazi kwa wataalamu wote wa sekta ya afya kwa sababu madai yao waliyajadili walipokutana na viongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat).
Waziri Mponda alisema anashangaa kuona madaktari hawakuafiki maelezo yao na wakatangaza mgomo. Nimuambie ukweli  Dk. Mponda kuwa inawezekana hawakuafiki au kuamini maelezo ya serikali kutokana na dola kuahidi mambo bila kutekeleza.
Mifano ipo mingi, kwa uchache angalia tatizo la malimbikizo ya mishahara na marupurupu ya walimu, serikali hivi sasa inajifanya haioni, walimu wakilipuka, viongozi wa serikali au wizara husika wataanza kuhaha kutafuta suluhu.
Wote tujiulize, kwa nini kunakuwa na malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa serikali wakati kila mwaka bajeti yao inasomwa na kupitishwa bungeni?
Hizo fedha zinakwenda wapi? Hapa kuna tatizo ambalo  sasa kisemeo cha wananchi yaani Bunge kupitia kwenye kamati yake husika inabidi waangalie hili. Anayesababisha haya awajibishwe maana anaitia aibu serikali nzima.

    No comments:

    Post a Comment