UGONJWA WA AJABU WAMTESA MAMA HUYU
Beatrice almaarufu MC Kimbaumbau, mkazi wa Kibamba wilayani Kinondoni yupo kitandani akiwa hajui hatima ya maisha yake kutokana na tatizo alilonalo la kuvimba mguu.
Akisimulia tatizo lake, Beatrice anasema:
“Nilianza kuumwa mwaka 1998, nilikuwa na shughuli zangu ambazo zilikuwa zikiniingizia kipato na kunifanya nimudu kusomesha watoto wangu.
“Tatizo la kuumwa mguu lilianza wakati natoka kazini, nilisikia kitu kama ganzi katika mguu huu wa kulia na baadaye ikaja homa kali, kitu ambacho kilinishangaza sana kwani sikuwahi kuumwa hivyo.
“Nilikwenda kutibiwa katika hospitali moja iliyopo Kimara na wakati nikiwa kituoni kusubiri usafiri, mguu ulianza kuvimba, hali ambayo ilinifanya nifikirie kuwa ni masuala ya kishirikina.
“Nilipofika nyumbani, baada ya siku chache mguu ulianza kutoka malengelenge kama mtu aliyeungua moto na ndipo vidonda vilipoanza kutoka.
“Nilipelekwa Hospitali ya Hindu Mandal kutibiwa vidonda hivyo lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya hadi ndugu zangu wakaamua kunipeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Madaktari katika hospitali hiyo, baada ya uchunguzi waliniambia mishipa inayotembeza damu mguuni imeziba lakini mfupa wa ndani uko salama.
“Kwa sasa siwezi kujishughulisha na chochote, huwa nalala tu, nikikaa nasikia maumivu makali sana, hakika sina raha ya maisha.
“Nimetibiwa sana sehemu mbalimbali lakini sipati nafuu, mawazo yangu sasa ni kwenda India kutibiwa lakini niliambiwa gharama yake ni shilingi milioni 45, yaani nauli na matibabu. Fedha hizo ni nyingi sana, mimi na ndugu zangu hatuna uwezo.
“Nina mtoto wangu ambaye alikuwa kidato cha pili, ameshindwa kwenda shule kwa kuwa sina fedha za kumlipia ada, hivyo tatizo hili limezaa tatizo lingine.
“Hivi sasa mtoto huyo kazi yake kubwa ni kuniogesha na kunipikia chakula kinapopatikana na kama hakipo tunalala njaa.
“Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie kunichangia chochote. Naamini kwa msaada wao nitaweza kupelekwa India na kutibiwa hadi kupona kwa sababu madaktari wa Muhimbili wamenithibitishia kuwa mfupa wangu ni mzima kabisa. Naumia sana mwenzenu,” alisema mama huyo huku akitokwa na machozi.
Mtu yeyote aliyeguswa na habari hii na anahitaji kumsaidia, anaweza kuwasiliana kwa simu yake namba 0716 850 350 au kutumia chochote kwa Tigo Pesa au kwa kutumia akaunti ya CRDB Namba 0112003893000 .
BFTZ SHARING IS CARING
No comments:
Post a Comment