Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam jana.
UAMUZI wa Serikali kuwaondoa vigogo wawili wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, umefanya madaktari ambao kwa mwezi mmoja walikuwa kwenye mgomo, wakubali kurudi kazini kuanzia Ijumaa.
Viongozi hao ni Katibu Mkuu, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa, ambao wamepewa likizo ya lazima, ili kupitisha uchunguzi wa tuhuma zilizochangia madaktari hao kugoma. Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipozungumza na wafanyakazi wa sekta ya afya, Dar es Salaam jana. Kwa upande wa Waziri, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya, Waziri Mkuu alisema watawajibishwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wowote.
Pamoja na uamuzi huo, Serikali pia ilitangaza kukubali madai yote nane ya madaktari ambayo yaliwafanya wagome. Pinda aliwaambia kuwa baadhi ya madai yatatekelezwa ndani ya muda mfupi na mengine yatalazimika kusubiri bajeti ijayo.
Akielezea kuondolewa kwa viongozi hao, awali Pinda alitaja baadhi ya tuhuma ambazo zinakabili watendaji hao wakuu wa wizara, kuwa ni kujitwalia zabuni ya kushona sare za watumishi wa sekta ya afya kwa gharama kubwa wakati hazina viwango. Tuhuma zingine ni kufanya ubadhirifu katika uagizaji vifaa vya kupimia virusi vya Ukimwi, ambao unasadikiwa kuwa viongozi hao walishiriki kupindisha taratibu, ili wafaidike na uagizaji wa vifaa bandia.
“Tumesikia hata mradi huu wa kusafisha bustani za hapa Muhimbili unamilikiwa na hawa viongozi…kwa kweli tuhuma zilizopo hazifurahishi hata kidogo,” alisema Pinda na kusisitiza
kuwa ndiyo maana wameamua kuwapumzisha. Pia viongozi wa wizara hiyo wanalalamikiwa kuwa jeuri na kwamba hawashughulikii kero za madaktari.
Malalamiko mengi yalikuwa yanaelekezwa kwa Katibu Mkuu Nyoni ambaye madaktari walidai anawadharau na wanapompelekea shida zao huwajibu kwa jeuri. Waziri Mkuu alisema wameamua kuwaondoa kwa nia njema kupisha vyombo vya Dola kufanya uchunguzi na kutafuta ukweli wa tuhuma zinazowakabili. “Nia ni kusafisha wizara na jina la wizara, tutawapa barua za likizo, halafu tuangalie kama kweli ni wachafu au ni wasafi...kwa kweli hatuna ujanja, ni lazima tuwapumzishe,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kwa upande wa viongozi wa kisiasa, “tulichofanya hili ni la ngazi ya kiteundaji … tumemwachia Rais aliyewateua alishughulikie…kwa ujumbe huu mtakuwa mnajua tunakoelekea ni wapi? Lengo letu ni kuleta picha nzuri pale wizarani ili kiongozi atakayepelekwa hapo akute ni pasafi.” Madai ya madaktari Pinda katika mazungumzo yake, alisema amelazimika kuunda Tume ya watu tisa ili kupitia na kutoa mapendekezo juu ya madai ya madaktari.
Alisema Tume hiyo ambayo imepewa wiki mbili, imeanza kuyafanyia kazi madai hayo na kutoa suluhisho. Alitaja madai ya kulipwa posho kwa madaktari walioko mafunzoni ambao ndio wanafanya kazi kubwa ya kushughulikia wagonjwa kabla ya kuonwa na madaktari bingwa. Alisema hilo tayari Serikali imewalipa madaktari hao; licha ya kuwa miezi miwili iliyopita hawakulipwa fedha hizo.
Kuhusu posho ya kuitwa kazini baada ya saa za kazi, ambayo madaktari wanadai iongezwe kutoka Sh 10,000 wanazolipwa sasa. Pinda alisema watapandisha posho hizo. Alisema kuanzia mwezi huu madaktari bingwa watalipwa Sh 25,000, wasio bingwa Sh 20,000 na wenye Stashahada watalipwa Sh 15,000 na watumishi wa kada zingine Sh 10,000. Madai ya posho ya kazi katika mazingira hatarishi, Pinda alisema wameiagiza hiyo timu kutoa mapendekezo
na kutambua ni makundi yapi yalipwe posho hiyo na kiasi cha fedha anachotakiwa kulipwa daktari.
Posho ya usafiri, Pinda alisema Serikali imekubali kuwakopesha madaktari wote mikopo ya kununulia magari, ili yawasaidie kwenda na kurudi kazini kama inavyofanya kwa watumishi wengine. Alisema hilo linaweza kutekelezwa mara moja ila akawaonya wasinunue magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser V-8 kwamba yatawaumiza. Kuhusu posho ya nyumba ambayo madaktari walitaka walipwe asilimia 30 ya mishahara yao, Pinda alisema kwa madaktari ambao hawana nyumba za Serikali watalipiwa pango.
“Hili tuna wajibu wa kulipia pango, ila kwa sasa siwezi kusema ni kiasi gani, kwani ni lazima tupige bajeti ya suala hilo.” Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu, Pinda alisema Serikali imekubali na itatekeleza kwa kuangalia ni madaktari wa maeneo yapi wanatakiwa kulipwa posho hiyo. Kuhusu madai ya ongezeko la mishahara hadi Sh milioni 3.5 kwa mwezi, Pinda alisema hilo si la madaktari peke yao, bali ni la watumishi wote wa sekta ya afya na akaonya kuwa lina athari kwa idara zote za Serikali.
Hata hivyo, aliahidi kupandisha mishahara katika bajeti ijayo, lakini si kwa kiasi hicho. “Iwapo tutakubali kulipa kiasi hicho, sekta ya afya peke yake mtakuwa mnatumia Sh trilioni 2 na sekta zingine zilizobaki kwa ujumla wao, ndizo zitatumia Sh trilioni moja kwa mishahara, hii si sawa kabisa. “Katika hili ni lazima niwe mkweli, hiyo pesa hatuwezi kuipata katikati ya bajeti hii, hapa tunachofanya ni kutekeleza kile kinachowezekana, hili la mishahara ni pana na ni gumu na zaidi tutaliangalia katika bajeti ijayo,” alisema Pinda.
Madai mengine ni ya bima ya afya ambayo walitaka madaktari wote wawe na kadi za kijani za Mfuko wa Bima ya Afya madai ambayo Pinda aliagiza yashughulikiwe haraka na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Kuhusu upatikanaji wa vifaa, Pinda alisema ameiagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kukopa vifaa kutoka Bohari ya Dawa ili kuhakikisha hospitali hiyo kuu ya Taifa inakuwa na dawa za kutosha na vifaa vinavyohitajika kwa daktari anapokuwa kazini.
Kurudi kazini Baada ya kueleza kilichofanywa na Serikali katika kushughulikia madai yao, Pinda aliwasihi madaktari hao kurejea kazini wote na akaahidi kuwa hakuna daktari hata mmoja atakayefukuzwa kazi. “Kipindi kile niliwaomba mrudi kazini, hamkutekeleza, kwani mlikuwa mnasaini vitabu na kuondoka. Leo nimerudi tena … madaktari wangu nawasihi toka rohoni, chonde chonde, nawaomba wote rudini kazini tukahudumie Watanzania.
“Cha msingi hapa ni wagonjwa. Hii ndiyo rai yangu kubwa kwenu leo hii. Nasikia ile kauli yangu ya kuwataka wanajeshi waje hapa iliwaudhi, jamani kile kilikuwa kitu cha mpito tu, hata leo wanaweza kurudi walikotoka, maana nao yale magwanda yao yanatisha. “Dhamira ya Serikali ni kuona mambo haya tuliyosema tunayatekeleza hatua kwa hatua. Naomba
muongozwe na kiapo chenu kama Watanzania na muwe na moyo wa huruma kwa wagonjwa, kwani hali ni mbaya.
“Hatuna dhamira yoyote ya kumfukuza daktari yeyote, ila dhamira yangu ni wagonjwa wapate huduma yenu, nawasihi wote rudini tukapate huduma yenu na Watanzania watawashukuru.” Uamuzi wa madaktari Baada ya kikao hicho na Waziri Mkuu na kuuliza maswali mengi juu ya hatma na matatizo yanayoikabili sekta ya afya, hatimaye madaktari hao katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati yao, Dk Steven Ulimboka, walikubali kurudi kazini kuanzia leo.
Pamoja na kukubali huko, madaktari hao waliazimia kuwa kati ya wiki mbili na mwezi mmoja, Serikali iwe imetekeleza mambo yanayohitaji utekelezaji wa haraka. Pia waliahidi kupeleka daktari mwenzao katika timu ya Waziri Mkuu inayoshughulikia madai yao. Madaktari hao walisema licha ya madai mengine kuelezwa kuwa yatatekelezwa katika bajeti ijayo, lakini walifurahi kuwa madai yao mengi yametekelezwa.
BFTZ SHARING IS CARING
No comments:
Post a Comment